Thursday, 22 March 2018

Waziri Mkuu Amuwaklisha Raisi John Magufuli Katika Mkutano Wa AU Rwanda
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa leo amemwakilisha Rais John Magufuli katika sherehe za kusaini mkataba wa kulifanya Bara la Afrika kuwa eneo huru la biashara jijini Kigali, Rwanda.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zaidi ya 50 ziilizosaini mkataba huo, ambao umeelezwa utaongeza chachu kwa Afrika kuimarika kiuchumi.

Mkataba huo umesainiwa baada ya kukamilika kwa kamati za wataalamu zilizoshirikisha pia mawaziri wa biashara na mambo ya nje wa nchi washirika.

Mbali na mkataba huo, marais hao pamoja na wawakilishi wa nchi washirika wamesaini Itifaki ya utekelezaji wa makubaliano hayo ambayo yanatoa uhuru wa makazi, kutembea, haki ya kuishi na kufanyakazi popote Afika bila vikwazo wala vizuizi sambamba na Tamko la Kigali.

Sherehe hizo pia zimehudhuriwa na Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi na Mwenyekiti wa CEO Round Table, Ally Mufuruki ambaye jana alikuwa miongoni mwa wazungumzaji katika mjadala wa uchumi na biashara.



Friday, 23 February 2018

Hiki ndicho Walichoongea Rais Magufuli na Kenyatta Baada ya Kukutana Leo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta wamewaagiza Mawaziri wa Tanzania na Kenya kutatua tofauti ndogondogo zinazojitokeza katika biashara kati ya nchi hizi mbili.

Marais hao wametoa maagizo hayo leo asubuhi tarehe 23 Februari, 2018 walipokutana na kufanya mazungumzo katika hoteli ya Munyonyo mjini Kampala muda mfupi kabla ya kuanza kwa vikao vya mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Kenyatta wamesema wanataka kuona biashara kati ya Tanzania na Kenya inazidi kukua na bidhaa zinauzwa na kununuliwa baina ya nchi hizo bila vikwazo vyovyote na hivyo kuagiza tofauti zilizojitokeza katika baadhi ya bidhaa zimalizwe.

“Kuna mambo madogomadogo yanakuwa yanajitokeza katika biashara kati ya Kenya na Tanzania, tunataka kwa haya yote Mawaziri wa Kenya na Mawaziri wa Tanzania mkae myatatue, sisi hatuna tatizo, mambo mengine madogomadogo mno, mambo ya viatu, nguo, ngano, gesi ni madogo sana, mnatakiwa myatatue nyinyi yasifike kwetu, sisi huku tuko sawasawa” amesema Mhe. Rais Magufuli na kuungwa mkono na Mhe. Rais Kenyatta.

Wametoa maagizo hayo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Balozi Monica Juma na Waziri wa Afrika Mashariki na Maendeleo ya Ushoroba wa Kaskazini wa Kenya Mhe. Peter Munya.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Sudani Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit katika hoteli ya Munyonyo Mjini Kampala.

Baada ya Mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki inaguswa na hali ya Sudani kusini na ametoa wito kwa pande zinazopingana kumaliza tofauti zao ili wananchi wa Sudani Kusini wajikite kujenga nchi yao.

“Nimemhakikishia Mhe. Rais Salva Kiir kuwa Tanzania ipo pamoja na Sudani Kusini na tunapenda tofauti zinazosababisha matatizo nchini mwake ziishe, sisi Tanzania tupo tayari kufanya biashara na Sudani Kusini, hata chakula kama wanahitaji tutawauzia” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Kwa upande wake Mhe. Rais Salva Kiir Mayardit amesema Tanzania na Sudani Kusini zina uhusiano wa kihistoria tangu enzi ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na kwamba japo kuna vita nchini mwake Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia kuwa uhusiano na ushirikiano huo utaendelezwa na kukuzwa zaidi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Gaston Sindimwo.

Mhe. Gaston Sindimwo amemfikishia ujumbe wa Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza kuwa hali ya Burundi ni shwari na Mhe. Rais Magufuli amesema anafurahi kuona sasa wakimbizi wa Burundi waliokuwa wamepata hifadhi Tanzania wameanza kurudi nchi kwao.

Mhe. Rais Magufuli pia amefanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa ambaye ni mratibu wa mazungumzo ya amani ya mgogoro wa Burundi aliyealikwa kuhudhuria mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hapa Kampala.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kampala
23 Februari, 2018

Saturday, 13 January 2018

Rais Kagame kufanya ziara nchini tarehe 14 Januari
 MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda amefunguka na kusema uwezo mkubwa wa Rais Magufuli na Demokrasia ya kweli ni jambo ambalo linawavutia wageni kuja Tanzania akiwepo Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame anayetarajiwa kuwasili nchini Jumapili.

Makonda amesema hayo leo akiwa katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam baada ya kuagana na Rais Magufuli ambaye ameelekea visiwani Zanzibar kushiriki sherehe za maadhimisho ya Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

“Amani Demokrasia ya kweli, upendo na uwezo wa mkubwa wa Rais Magufuli ndiyo msingi wa kuwavuta wageni kuja kutembelea hakuna mgeni ambaye anaweza kutembelea nchi ambayo haina upendo, amani na mshikamano. Tanzania chini ya uongozi wa Rais Magufuli inaendelea kuchanja mbuga katika nyanja za kidemokrasia hasa pia katika uwanja mwingine wa kidiplomasia na kuwafanya wageni waone sehemu nzuri ya kuja kutembelea,” alisema Makonda.

Mbali na hilo Makonda amesema kuwa Rais Paul Kagame atawasili nchini Tanzania siku ya Jumapili ya tarehe 14 ambapo atakuwa nchini kwa ziara ya siku moja na kufanya mazungumzo na Rais John Pombe Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam.
 

Friday, 12 January 2018

Kenya Airways yazindua safari za moja kwa moja hadi Marekani
Shirika la ndege la Kenya, Kenya Airways, limezindua uuzaji wa tiketi za safari ya kwanza kabisa ya ndege zake za moja kwa moja kutoka Nairobi hadi Marekani.

Shirika hilo linapanga kufanya safari yake ya kwanza mnamo 28 Oktoba, hatua itakayoifanya Kenya Airways kuwa shirika la kwanza kutoka Afrika Mashariki kuwa na safari za moja kwa moja Marekani.

Ndege za shirika hilo litakuwa zinafasiri moja kwa moja hadi uwanja wa ndege wa JFK, New York.

Tiketi za kawaida zinauzwa Sh89,000 ($890).

Mwenyekiti wa bodi ya Kenya Airways Michael Joseph
Kenya Airways itafanikisha safari hizo kwa ushirikiano na shirika la Delta Airlines la Marekani.
Mambo muhimu kuhusu safari hiyo:

    Safari hiyo itachukua saa 15 kutoka New York hadi Nairobi na saa 14 kutoka Nairobi hadi New York.
    Shirika hilo limesema litatumia marubani wanne na wahudumu 12 wa ndege.
    Safari yote itatumia tani 85 za mafuta.
    Shirika hilo litatumia ndege zake za kisasa aina ya Boeing 787 Dreamliner ambazo huwabeba abiria 234.
    Ndege za kwenda Marekani zitaondoka JKIA Nairobi saa 23:25 na kufika JFK kesho yake saa 06:25.
    Ndege za kurudi Nairobi zitaondoka New York 12:25 na kutua JKIA saa 10:55 kesho yake.

Masharti

Kwa mujibu wa Bodi ya Utalii Kenya, Kenya hupokea watalii 100,000 kutoka Marekani kila mwaka na safari hizo zinatarajiwa kuifanya nafuu kuzuru Kenya kwa kupunguza muda wa kusafiri na gharama.
Kuzinduliwa kwa safari hizo ni matunda ya mashauriano ya muda mrefu kati ya Kenya na serikali ya Marekani.

Kenya ilipewa masharti ya kuimarisha usalama, ikiwa ni pamoja na kuwatenganisha abiria wanaotua na wanaoondoka, kufanya salama njia za safari ya ndege na pia kuweka ua katika uwanja wa ndege wa JKIA.

Kenya ilipewa hadi ya Kiwango cha Kwanza kutoka kwa Shirika la Safari za Ndege la Marekani Februari mwaka jana na kuifungulia njia Kenya Airways kufanya safari za moja kwa moja.

Thursday, 11 January 2018

Kenya yakasirishwa na ripoti ya EU kuhusu uchaguzi uliopita
.erikali ya Kenya imekasirishwa na ripoti iliotolewa na kiongozi wa Muungano wa Ulaya kuhusu uchaguzi mkuu wa urais mwaka uliopita.

Marietje Schaake alitoa ripoti mapema siku ya Jumatano katika mji mkuu wa Ubelgiji , Brussels baada ya kusema kuwa serikali ya Kenya haikuwa tayari kukutana naye.

Taarifa kutoka ubalozi wa Kenya mjini Brussels inasema kuwa madai hayo sio ya ukweli na kwamba alikiuka makubaliano kati ya taifa hilo na EU.
Taarifa hiyo iliendelea kusema kwamba mpango wa kuzuru taifa hilo ulikubaliwa kati ya katikati ya mwezi Februari hadi katikati ya mwezi Machi.
Bi Schaake alisema katika taarifa yake kwamba alikuwa anatoa ripoti hiyo ya kuafikia sheria za muungano huo za kutoa ripoti miezi mitatu baada ya uchaguzi.

Ripoti hiyo inaangazia wasiwasi kuhusu utumizi wa mali ya umma na vitisho dhidi ya maafisa wa uchaguzi wakati wa uchaguzi huo uliokumbwa na utata.
Inatoa mapendekezo 29 kuhusu vile mfumo wa uchaguzi wa Kenya unavyoweza kuimarishwa, lakini bi Schaake aliambia BBC kwamba ni Wakenya wenyewe wanaoweza kutatua tatizo hilo.

Rais Uhuru Kenyatta alichaguliwa katika uchaguzi wa marudio mnamo mwezi Oktoba ambao ulisusiwa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Uchaguzi wa kwanza uliofanyika mnamo mwezi Agosti, ambao bwana Kenyatta aliibuka mshindi ulifutiliwa mbali na mahakama ya juu.

Uchaguzi huo ulikumbwa na ghasia huku makundi ya haki za kibinaadamu yakisema kuwa takriban watu 50 wengi wao wakiwa wafuasi wa upinzani waliuawa na maafisa wa polisi.

Maafisa wa polisi hatahivyo wamepinga madai hayo.

Wednesday, 10 January 2018

Mwalimu wa shule ya msingi mwenye umri wa miaka 24 anashikiliwa na jeshi polisi baada ya kumuua kwa kumchoma kisu mume wake mwenye umri miaka 25 kwa madai ya kumyima tendo la ndoa nchini Uganda.

Harriet Nambi inasemekana amemuua Musa Batera kwa kukataa kushiriki naye tendo la ndoa kwa miezi miwili baada ya kujifungua kwa njia ya upasuaji.

Majirani zake wamesema, Nambi alikuwa analalamika kwamba mumewe ameshindwa kumtimizia  mahitaji yake ya ndoa licha ya yeye kumueleza mara nyingi kuwa anahitaji.

Nambi alitishia kumfanyia kitu kibaya mumewe ambaye ni dereva wa bodaboda na aliporejea nyumbani jioni ugomvi uliibuka na akachukua kisu na kumchoma hadi akafariki. Mwanaume huyo  ana wake wengine wawili.

Nambi amekamatwa na polisi wa Uganda na yupo kizuizini akisubiri mashtaka kuhusu mauaji. Mwili wa Batera ulikabidhiwa ndugu zake kwa mazishi.

Tuesday, 9 January 2018

Watu 30 walazwa hospitalini Mombasa kutokana na ugonjwa wa chikungunya
Watu 30 wamelazwa kwenye hospitali mbali mbali za kaunti ya Mombasa pwani mwa Kenya baada ya kuugua ugonjwa wa Chikungunya, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali KBC.

Gavana wa Mombasa Hassan Joho, amezindua magari matano yenye mashine na dawa kunyunyisiwa katika kaunti hiyo wakati ugonjwa unazidi kuwatishia watu zaidi.

Chini ya miezi mitatu iliyopita kaunti ya Mombasa ilikuwa ikikabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambapo watu kadha walilazwa hospitalini na maeneo kadhaa ya mankuli kufungwa katika kaunti hiyo.
Joho alithibitisha kuwa kumekuwa na visa 120 vya wagonjwa na imethibitwa kuwa visa 32 kati ya hivyo ni vya ugonjwa wa chikungunya.

Kufuatia ugonjwa huo kusambazwa na mbu Gavana Joho amewashauri wenjeji wa mombasa kushirikiana kwa karibu na serikali ya kaunti kuondoa mazingira salama kwa mbu.

Thursday, 4 January 2018

Barua aliyoipokea leo Rais Magufuli toka kwa Rais Museveni
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 04 Januari, 2018 amepokea barua kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni iliyowasilishwa na Mjumbe Maalum Mhe. Sam Kutesa ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda.

Pamoja na kupokea barua hiyo Mhe. Rais Magufuli amefanya mazungumzo na Mhe. Sam Kutesa, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Baada ya mazungumzo hayo Mhe. Sam Kutesa amesema Mhe. Rais Museveni amemtumia Mhe. Rais Magufuli na Watanzania wote salamu za heri ya mwaka mpya na pia wamezungumzia masuala yahusuyo uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda.

Mhe. Sam Kutesa amesema Uganda inafurahishwa na kuridhishwa na uhusiano na ushirikiano mzuri na wa kindugu uliopo kati yake na Tanzania na kwamba mazungumzo ya leo yalijikita kuuimarisha zaidi kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.

“Tumezungumza namna tutakavyoimarisha na kukuza zaidi uhusiano wetu katika maeneo mbalimbali, kama unavyojua kuna miradi ya maendeleo ya ushirikiano ukiwemo mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga hapa Tanzania, na miradi mingine na masuala mbalimbali ya ushirikiano” amesema Mhe. Sam Kutesa.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Januari, 201

Wednesday, 3 January 2018

Wanyarwanda Kutotambulika kama Wakimbizi
Mataifa mbalimbali duniani, hayatawatambua tena raia wa Rwanda waliokimbia nchi yao kati ya mwaka 1959 hadi 1988 kama wakimbizi baada ya muda waliopewa kurudi nyumbani kumalizika mwisho wa mwaka 2017.

Hatua hiyo inaamanisha kuwa, raia hao wa Rwanda hawatatambuliwa kama wakimbizi na hawatapa msaada wowote kutoka kwa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR.

Disemba 31 mwaka jana, ilikubaliwa kati ya serikali ya Rwanda na Shirika la UNHCR pamoja na mataifa mbalimbali ambayo yamekuwa yakiwapa hifadhi wakimbizi hao kutoka Rwanda warejee nyumbani.

Mkataba wa kurejesha nyumbani wa wakimbizi uliokubaliwa mwaka 1951, unawataka wakimbizi kurejea katika nchi zao baada ya kubainika kuwa, hawapo tena katika hatari ya kushambuliwa au kunyanyaswa.

Wanyarwanda wanaoishi nje ya nchi yao ambao wamekuwa wakifahamika kama wakimbizi ni takriban elfu 20 kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.

Tuesday, 2 January 2018

UGANDA: Rais Museveni aidhinisha sheria kuondoa kikomo cha umri wa rais
Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameidhinisha mswada unaoondoa kikomo cha umri kwa wagombea urais nchini humo, hatua inayompa nafasi ya kuwania tena urais mwaka 2021.

Mswada huo pia unarejesha takwa la rais kuongoza kwa mihula miwili pekee ya miaka mitano.

Kwa kuwa sheria hiyo itaanza kutekelezwa sasa, Bw Museveni anaweza akaongoza taifa hilo hadi 2031.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la Uganda, katibu wa rais Bi Linda Nabusayi amesema Bw Museveni alitia saini mswada huo kuwa sheria Desemba 27 na kisha akatuma waraka tarehe 29 Desemba.

Sheria ya awali ilikuwa inamzuia mgombea kuwania urais baada ya kutimiza umri wa miaka 75. Bw Museveni kwa sasa ana miaka 73.

Hatua ya rais huyo kuidhinisha mswada huo imetoa wakati ambao amekuwa akihimizwa na viongozi wa kidini na wanaharakati wa kisiasa kutouidhinisha.

Bunge liliidhinisha mswada huo mnamo tarehe 10 Desemba kwa zaidi ya theluthi mbili ya wabunge waliohudhuria kikao, wabunge 317 wakiunga mkono na 97 wakapinga.

Chanzo; BBC

Monday, 1 January 2018

Rais Magufuli amtumia salamu za rambirambi Rais wa Kenya kufuatia ajali ya barabarani
Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kutokea kwa ajali iliyosababisha ndugu zetu takribani 36 kupoteza maisha baada ya basi la abiria kugongana na roli katika barabara ya Nakuru - Eldoret nchini Kenya.

Msiba huu umesababisha majonzi makubwa sio tu kwa ndugu zetu wa Kenya bali pia kwetu sote wana Jumuiya ya Afrika Mashariki, tumepoteza wapendwa wetu na nguvu kazi yetu.

Kwa niaba ya Watanzania wote nakupa pole sana ndugu yangu Mhe. Uhuru Kenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya kwa msiba huu mkubwa ulioupata, nawapa pole wana familia wote waliowapoteza jamaa zao na pia nawapa pole wananchi wote wa Kenya.

Naungana nanyi katika kipindi hiki kigumu cha majonzi, nawaombea majeruhi wote wa ajali hii wapone haraka na Marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi, Amina".

Hizi ni salamu za rambirambi alizozitoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta kufuatia ajali ya barabarani iliyosababisha vifo vya watu takribani 36 baada ya basi la abiria kugongana na roli katika barabara ya Nakuru - Eldoret nchini humo tarehe 31 Desemba, 2017.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
31 Desemba, 2017


Wednesday, 27 December 2017

Rwanda kupiga Kura juu ya Kanuni za Makosa ya Jinai
 Kigali, mji mkuu wa Rwanda

Wabunge nchini Rwanda wiki hii wataanza kupigia kura mswada mpya unaoeleza kanuni mpya za makosa ya jinai nchini humo.
Serikali, kupitia Tume ya Marekebisho ya Sheria ya Rwanda, ilianza kuchunguza kanuni mpya za makosa ya jinai za mwaka 2015 kama sehemu ya jitihada za kurejelea kuweka sawa mfumo sheria za makosa ya jinai nchini humo.
Serikali imekuwa ikibadilisha sheria hiyo tangu mwezi Oktoba mwaka huu.
Wizara ya Katiba na Sheria nchini humo inasema, lengo la mabadiliko hayo ni kufanya sheria hiyo kueleweka kwa urahisi na kukabiliana vilivyo na makosa mbalimbali.
Waziri wa Katiba ya SheriaEvode Uwizeyimana aliwaambia wabunge kwamba mabadiliko yaliyopendekezwa yanalenga kuifanya raihisi sheria ya makosa ya jinai katika kuitumia na nuifanya ngumu kwa kukomesha uhalifu, kuadhibu wale wote watakaopatikana na uhalifu huo na kukabiliana na wahalifu.
Katika mahojiano ya simu na gazeti la New Times jana Jumanne , Mbunge John Ruku-Rwabyoma alisema kama wabunge wenzake walikubaliana kuhusu ibara zote, Wanyarwanda watashuhudia mabadiliko mengi na watafurahi
Amebaini kwamba sheria kuhusu utoaji mimba, huenda ikakubaliwa na wabunge wenzake na, hii itakua ni hatua nzuri.

Tuesday, 26 December 2017

TUNDU LISSU ASIMAMA KWA MARA YA KWANZA HOSPITALINI
Mwanasheria mkuu wa chama upinzani Chadema nchini Tanzania Tundu Lissu, ameweza kusimama kwa mara ya kwanza baada ya kushambuliwa.

Tundu Lissu amekuwa akipokea matibabu Nairobi tangu alipopigwa risasi na watu wasiojulikana jijini Dodoma mwezi Septemba.

Katika picha iliowekwa katika ukurasa wa Facebook wa CHADEMA, mbunge huyo anaonekena akisimama akisaidiwa na wahudumu wawili wa hospitali.

Ujumbe ulioambatana na picha ukisema "Wiki iliyopita niliwataarifu kwamba madaktari wangu wamesema 'nitasimama, nitatembea na nitarudi Tanzania.Leo Boxing Day (Tarehe 26 Disemba) nimeweza kusimama kwa mguu mmoja kwa msaada wa 'Mababa Cheza' wangu. Hatua inayofuata ni magongo kesho na nitawajulisheni hatua nyingine katika matibabu yangu."
Bwana Lissu ambaye pia ni mkuu wa chama cha mawakili nchini Tanzania amekuwa akizozana na serikali ya Rais Magufuli na alikamatwa mara sita mwaka huu pekee, akishtumiwa kwa kumtusi kiongozi huyo wa taifa mbali kuharibu usalama wa umma, miongoni mwa mashtaka mengine.amesema anaamini kushambuliwa kwake kulihusiana na siasa nchini humo.

Akizungumza na BBC hivi karibuni mbunge huyo wa Singida Mashariki amelilaumu Bunge la nchi hiyo akisema halijachukua hatua zozote kumsaidia tangu kulazwa kwake hospitalini.

Makamu wa Rais wa Tanzania Bi Samia Suluhu alimtembelea hospitalini mwezi Novemba.

Sunday, 24 December 2017

Upelelezi juu ya Mauaji ya Kimbari Rwanda Umekamilika..........Kagame Naye Katuhumiwa Kuhusika
Majaji nchini Ufaransa wamewalaumu wapiganaji walioongozwa na Rais wa sasa wa Rwanda, Paul Kagame kwa kuilenga na kuiangusha ndege iliyokuwa imembeba Rais wa wakati huo wa Taifa hilo, Juvenal Habyarimana 1994.

Hii ni baada ya upelelezi juu ya suala hilo kukamilika. Upelelezi huo ulikuwa unafanywa na Majaji hao wa Ufaransa juu ya shambulio la kombora lililosababisha kifo cha Rais Habyarimana na baadaye kusabisha kuanza kwa mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka huo huo.

Hata hivyo Rwanda nayo inawalaumu Ufaransa kwa kushiriki kupanga mauaji ya kimbari.

Upelelezi huu umesababisha mitafaruku kati ya Rwanda na Ufaransa jambo lililosababisha kuvunja uhusiano wao wa kidiplomasia mwaka 2006.

Thursday, 21 December 2017

Uganda yaondoa Kikomo cha Umri wa kugombea Urais



Rais Yoweri Museveni

Wabunge wa Uganda wameyapitisha mabadiliko ya Katiba ambayo sasa yanamruhusu Rais wa sasa Yoweri Kaguta Museveni kuwania nafasi hiyo ya juu kabisa kwa muhula wa sita.
Baada ya siku tatu za majadiliano mazito na mivutano, hatimaye waondoa ukomo wa umri wa miaka 75 kwa mgombea urais. Wabunge wa upinzani walitoka ndani ya ukumbi zaidi ya mara moja na sita kati yao walifukuzwa ukumbini kutokana na kuupinga muswada. Na hatimaye spika wa bunge hilo Bi Rebecca Kadaga akitangaza matokeo baada ya kupiga kura ya mwisho ikiwa wapiga kura wawili hawakuwa na upande, upinzani wamepata kura 62 na wanaotaka kuondowa kikomo kura 315 na hivyo Spika kutangaza kuwa mswaada huo umepita baada ya kusomwa mara ya tatu.
 Wabunge wa Uganda

Wabunge pia wamerejesha ukomo wa vipindi viwili vya kukaa madarakani kutoka miaka saba hadi miaka mitano, kwa hivyo wabunge wa sasa wataendelea kuongoza hadi mwaka 2023.
Ni pengine kutokanana malalamiko kuwa kuondolewa kwa ukomo wa umri kunaweza kumfanya Bwana Museveni kuwa Rais wa milele. Wafuasi wa Museveni wanadai ni waganda ndiyo wanaweza kumwondoa madarakani kwa Kura.
Upande wa upinzani waliweka pingamizi kuzuia mswaada huo usipite lakini idadi yao katika bunge ni ndogo, kiongozi wa wabunge wa upinzani Winne Kiiza amesikitishwa na kupitishwa mswaada huo.
Lakini upande wa chama tawala ulitumia kila mbinu kuona kwamba mswaada huo unapita ili Rais Museveni kuendelea kutawala .
Kupitishwa mswaada huo kunampatia tena Rais Museveni kutawala miaka mingine 14 kulingana na mswaada huo, lakini raia wa Uganda wengi walikuwa hawaungi mkono kubadilishwa kwa katiba kumuongeza Rais Museveni kutawala baada ya kutawala zaidi ya miongo mitatu.

BBC SWAHILI)(



Monday, 18 December 2017

Kimbisa ajitosa kugombea Uspika wa Bunge la EALA.
Adam Kimbisa.
Wateule wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) wanaowakilisha nchi zao ndani ya Jumuiya hiyo, wanatarajia kuapishwa na pia kuchagua Spika mpya wa bunge hilo, katika kikao cha Bunge hilo, kinachoanza jijini Arusha leo.
Kwa upande wa Tanzania, Adam Kimbisa amejitokeza kuwania nafasi hiyo akichuana na Leontine Nzeyimana (Burundi) na Martin Ngoga (Rwanda). Hatua hiyo, itatanguliwa na wabunge hao kwanza kuapishwa rasmi mbele ya Katibu wa Bunge hilo kuwa wabunge wa Bunge hilo.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Bunge hilo, Bobi Odiko, Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, anatarajiwa kuhudhuria uchaguzi huo pamoja na maspika wenzake kutoka nchi za jumuiya hiyo wa Kenya, Rwanda, Uganda, Burundi na Sudan Kusini.
Spika mpya wa EALA atakayechukua nafasi ya aliyekuwa spika wa Bunge hilo, Daniel Kidega, anatarajiwa kuongoza chombo hicho kwa miaka mitano ijayo. Nchi zote sita wanachama wa EAC zimewasilisha majina nane ya wabunge wanaoziwakilisha ndani ya Bunge hilo kwa Bunge hilo lenye makao yake makuu, jijini Arusha.
Ajenda kuu katika Bunge hilo, ni uapisho wa wabunge wapya, uchaguzi wa spika na uapisho wa wajumbe wa Kamisheni ya EALA na uteuzi wa kamati mbalimbali. Bunge hilo, lilitarajiwa kuanza vikao vyake tangu Juni 4, mwaka huu na kumalizika Juni 5, mwaka huu lakini ilishindana baada ya nchi tatu tu ambazo ni Uganda, Tanzania na Burundi kukamilisha taratibu zote.
Nchi ya Sudan Kusini ambayo kwa sasa Bunge lake ni la mpito ilibidi lirejee tena uchaguzi wake wa wabunge wa Afrika Mashariki baada mmoja wa wananchi wa nchi hiyo, Wani Salantino kukata rufaa katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) kupinga utaratibu mzima wa uchaguzi huo.
Kutokana na hatua hiyo, Bunge hilo la Sudan Kusini ilibidi lirejee tena uchaguzi huo, Agosti 3, mwaka huu na kuwasilisha majina ya wabunge waliochaguliwa kuiwakilisha nchi hiyo EALA.
Uganda ilikuwa ndiyo nchi ya kwanza kufanya uchaguzi wa wabunge wa EALA Machi Mosi, mwaka huu na wabunge waliochaguliwa ni pamoja na Susan Nakawuki, Fred Mukasa Mbidde na Chris Opoka.
Wengine ni Rose Akol, Mathias Kasamba, Mary Mugyenyi na Hon Paul Musamali. Dennis Namara, na George Stephen Odongo. Bunge la Tanzania lilimrejesha aliyekuwa mbunge wa EALA, Adam Kimbisa na Maryam.
Wabunge wengine wapya wa EALA wanaoiwakilisha Tanzania ni Josephine Lemoyan, Happiness Lugiko, Pamela Maassay, Dk Ngwaru Maghembe, Dk Abdullah Makame, Habib Mnyaa na Fancy Nkuhi.
Kwa upande wa Rwanda wabunge wanaoiwakilisha nchi hiyo EALA ni Pierre Celestin Rwigema, Martin Ngoga, Gasinzigwa Oda, Kalinda Francois Xavier, Alex Bahati, Fatuma Ndangiza, Rutazana Francine, Barimuyabo Jean Claude na Uwumukiza Francoise.
Aidha, kwa upande wa Burundi, wabunge wa Afrika Mashariki wanaowakilisha nchi hiyo ni Jean Marie Muhirwa, Leontine Nzeyimana, Ahingejeje Alfred, Burikukiye Marie Claire, Burikukiye Victor, Karerwa Mo-Mamo, Nduwayo Christophe, Rurakamvye Pierre Claver na Nsavyimana Sophie.
Wabunge wa Sudan Kusini ni Dk Ann Itto Leonardo, Gai Deng Nhial Deng, Dr Woda Jaremiah Odok, Gabriel Garang Ahol, Dk Gabriel Garang Arol, Thomas Deng, Mukulia Kennedy Ayason, Kim Duop na Gideon Gatpan Thoar. Bunge la Afrika Mashariki ni chombo cha jumuiya hiyo kilichoanzishwa mwaka 2001 kikiwa na hadhi ya Bunge lenye wawakilishi wa nchi zote wanachama

Thursday, 14 December 2017

RAIS WA MSUMBIJI AWASILI NCINI LEO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Rais wa Msumbiji Mh. Filipe Nyusi alipowasili mjini Dodoma. PICHA NA IKULU.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpokea Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa mjini Dodoma. PICHA NA IKULU,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi katika Ikulu ya Dodoma kabla ya kuanza mazungumzo yao. PICHA NA IKULU.